Magaidi Quotes

Quotes tagged as "magaidi" Showing 1-8 of 8
Enock Maregesi
“Ujanja wote ulimwisha Murphy. Ilimbidi kutoboa siri ili adui asizidi kumuumiza. Alilaumu mno kufa wakati alishakula ng’ombe mzima. Alifikiri Mogens na Yehuda walishauwawa kulingana na hasira nyingi za magaidi. Walihakikisha hawafanyi makosa hata kidogo. Alivyomaliza kumhoji, yule adui alizunguka nyuma katika mgongo wa Murphy na kwenda katika dirisha lililokuwa wazi – la mashariki – ambapo aliegemea na kuvuta sigara. Alichungulia kidogo nje kisha akageuka na kuendelea kupata upepo mdogo wa baridi.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Nusu dakika baada ya kuondoa gari, Murphy aliona kiwiliwili cha mtu kikimwendea mbio kutokea katika nyumba ya magaidi! Hapohapo alisimamisha gari na kuacha taa zikiwaka, halafu akashika bunduki na kushuka – akiwa ameangalia mbele kwa tahadhari kubwa. Alikuwa mwanamke. Debbie! Murphy alipojua ni Debbie, alitupa bunduki na kuchomoka mbio mpaka wakakutana na kukumbatiana kwa nguvu! Murphy alimbeba Debbie na kumbusu kila sehemu, halafu akamfuta machozi na kumbembeleza.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Sigara zilizidi kuvutwa, ndani ya nyumba, na magaidi wale wawili, wakati Murphy akisinzia kudanganyia kama kweli nguvu zilishamwisha. Alimfikiria tena mpenzi wake Sophia, safari hii sana. Alimkumbuka Debbie; hakujua alikuwa wapi na hakujua mama yake angefanya nini kama Debbie angekufa, na Murphy ndiye aliyetoka naye. Debbie alimuuma zaidi. Alimkataza kufa kwa ajili ya mchumba wake. Sasa alikufa kwa ajili ya mtu ambaye hakumjua. Murphy alijilaumu kumtongoza na kumchukua kwao na kulala naye na kula chakula chake cha kifalme. Wazazi wake wangejisikiaje kama angekufa, tena katika mazingira ya kutatanisha kama yale. Kufa alijua angekufa; lakini Mungu angemsaidia, awaage watu wake.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Polisi wa kituo cha kati cha Coyoacán kumbe hawakuwa mbali na sehemu zile. Walipoona gari zikifukuzana waliona ujanja ni kuwakatisha Vijana wa Tume katika vichochoro. Haikuchukua muda magari sita ya polisi yalitokeza Vallarta (Barabara ya Vallarta) na kuliona gari la Vijana wa Tume Gómez Farías likipepea kwa mwendo mkali kuelekea Cuauhtémoc, na gari za magaidi kwa nyuma yao. Kwa vile Ferrari ilikuwa mbali kidogo na magari ya magaidi, polisi hawakuitilia maanani sana kwa kudhani yale mawili (ya magaidi) ndiyo yaliyokuwa yakifukuzana. Bila kuchelewa, magari mawili ya polisi yalikamata Hidalgo na kuzunguka mpaka Moctezuma halafu yakasimama ghafla katikati ya Moctezuma na Gómez Farías – katikati ya magari mawili ya magaidi na gari la Vijana wa Tume. Wakati huohuo magari mengine (manne) ya polisi yakitokea Mtaa wa Vallarta nayo yakasimama nyuma ya magari ya magaidi; hivyo kufanya magari ya magaidi yawe katikati ya magari ya polisi, na polisi wakaisahau Ferrari ya Lisa.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Kasoro za Uzi zilizofanya zisitumiwe tena na kikosi cha usalama cha rais wa Marekani ni kutokuwa na shabaha imara katika umbali mfupi (hutawanya risasi na huleta madhara makubwa katika umbali mfupi hivyo kuweza kudhuru hata watu wasiokuwa na hatia) na kutokuwa na uwezo wa kutoboa kinga ya risasi dhidi ya magaidi wanaotumia mavazi ya kuzuia risasi, wanaotishia usalama wa rais wa Marekani. Gaidi mwenye mavazi ya kuzuia risasi aliweza kumdhuru rais kwa maana ya USSS kushindwa kumdhibiti. Badala yake, sasa USSS wanatumia FNP90 – zenye uwezo wa kutoboa kinga ya risasi, na ambazo hazileti madhara makubwa katika umbali mfupi na katika umbali mrefu. Bunduki hizi, zenye uwezo wa kubeba risasi 100 katika chemba zake mbili za Kampuni ya Beta ('Century Magazines'), zilitumiwa na magaidi wa Kolonia Santita dhidi ya Vijana wa Tume na dhidi ya polisi wa Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“John Murphy alifika Moscow tarehe 1/11/1992 saa 11 alfajiri akitokea Cairo, Misri. Wakati huo Moscow kulikuwa na baridi sana. Teksi yake ilipofika Teatralny Proezd, upande wa kusini wa Hoteli ya Metropol – karibu na mojawapo ya minara ya mwanzo ya Kitay-gorod, kitovu kikuu cha biashara cha Moscow ya kale – kwa matatizo ya injini; magaidi wanne, waliokuwa wakimfuatilia kwa gari aina ya Bentley Continental S nyeusi – iliyokuwa na namba za kitemi za B 001 BB 77 RUS mali ya Kiongozi wa CS-Moscow Dmitri Olegushka – toka Uwanja wa Ndege wa Sheremetyevo II wa kaskazini-magharibi mwa jiji la Moscow, waliendelea mbele na kusimama mkabala na Jumba la Maonyesho ya Tamthilia la Bolshoy; kisha wawili kati yao wakashuka na kuingia ndani ya kioski, wawili wakibaki ndani ya gari kuhakikisha John Murphy hawapotei. Magaidi hao wa CS-Moscow, Tawi la Kolonia Santita la Urusi na nchi zote za Ulaya ya Mashariki na baadhi ya nchi za Ulaya ya Kusini, walijua Murphy alishawahisi.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“Kilometa mbili na ushei kidogo kutoka katika sanamu la Yesu Mtoto liitwalo Niñopa, katika Kanisa la Parokia ya Manispaa ya Xochimilco ('Sochimiliko') la Iglesia de San Bernardino de Siena, Mexico City, kulikuwa na nyumba ndogo ya siri ('safe house') ya Kolonia Santita iliyojengwa bila uzio wa ukuta au seng’enge isipokuwa miti iliyopandwa kuizunguka bila mpangilio wowote. Ndani ya nyumba hiyo Mpelelezi Maarufu Duniani John Murphy alikuwa akiteswa na magaidi kumi na mbili; waliokuwa wakiendelea kushangaa jinsi alivyookoka katika ajali ya ndege iliyoua watu zaidi ya mia tatu huko Uholanzi, na jinsi alivyoweza kuingia katika ofisi ya siri ya Panthera Tigrisi, kitu kilichomchanganya akili Tigrisi na makompade wote wa Kolonia Santita duniani kote. Bila Mtoto wa Rais wa Meksiko Debbie Patrocinio Abrego, na mwanasesere wa nyoka wa Mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Lisa Madrazo Graciano, John Murphy angeanguka.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“Kama George Bush angekuwa na amani ndani ya moyo wake na Saddam Hussein angekuwa na amani ndani ya moyo wake Vita ya Ghuba isingetokea. Vilevile, katika kitabu cha ‘Kolonia Santita’, kama Rais wa Tume ya Dunia angekuwa na amani ndani ya moyo wake na kiongozi wa Kolonia Santita angekuwa na amani ndani ya moyo wake Kolonia Santita isingepigana na Umoja wa Mataifa. Taifa lisingepigana na taifa, na mataifa yasingepigana na magaidi.”
Enock Maregesi