Aleksi Toth
Aleksi Toth (18 Machi 1854 - 7 Mei 1909) alikuwa padri wa Kanisa la Kiorthodoksi nchini Marekani.
Tangu mwaka 1994 anaheshimiwa na Waorthodoksi kama mtakatifu.
Sikukuu yake huadhimishwa katika tarehe ya kifo chake.
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Alizaliwa huko Kobylnice, leo nchini Slovakia, katika familia fukara ya Wakatoliki wa Mashariki katika Dola la Austria-Hungaria. Baba yake alikuwa padri, kama baadhi ya ndugu zao. Alipata malezi mazuri na kujifunza lugha mbalimbali. Baada ya kumuoa Rosalie Mihalich, alipata upadrisho tarehe 18 Aprili 1878, lakini mke na mtoto wao pekee walifariki mapema.
Miaka 1879-1889 alifanya kazi za karani wa askofu wa Presov, mwalimu seminarini n.k.
Mnamo Oktoba 1889 aliteuliwa kuwa paroko wa Wakatoliki wa Mashariki huko Minneapolis, Minnesota, Marekani. Huko aliripoti kwa askofu mkuu John Ireland, ambaye alikuwa kati ya waliotaka kufanya Wakatoliki wote wafuate mapokeo ya Roma na lugha ya Kiingereza. Hivyo askofu alimkataa, lakini padri Toth kama mtaalamu wa sheria za Kanisa alijua haki za Wakatoliki wa Mashariki.
Isitoshe, maaskofu wa Marekani walimuomba Papas awarudishe Ulaya mapadri wote wa Kanisa la Mashariki. Hapo mnamo Oktoba 1890, mapadri 8 kati ya 10 wa Kanisa hilo waliokuwepo Marekani walikutana huko Wilkes-Barre, Pennsylvania, padri Toth akiwa mwenyekiti wa kikao.
Askofu mkuu Ireland aliwaandikia waumini wake wasishiriki ibada za padri Toth, naye aliona afadhali kurudi Ulaya. Kumbe waumini walimuomba awasiliane na askofu wa Warusi Waorthodoksi, Vladimir. Baada ya mawasiliano kukamilika, askofu huyo alifika Minneapolis ambapo tarehe 25 Machi 1891 aliwapokea padri Toth na waumini wengine 361 katika Kanisa la Kiorthodoksi. Mfano huo ulifuatwa na wengine wengi, zikiwemo parokia 17 na waumini 20,000 kwa juhudi za padri Aleksi.
Alifariki huko Wilkes-Barre.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Watakatifu wa Agano la Kale
- Orodha ya Watakatifu Wakristo
- Orodha ya Watakatifu wa Afrika
- Orodha ya Watakatifu Wafransisko
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Alexis of Wilkes-Barre. Biography of St. Alexis Toth from the OrthodoxWiki website.
- Orthodox Christians in North America: 1792–1994, Chapter 2, contains info on Toth, including particulars of his conversation with Bishop Ireland.
- Ὁ Ἅγιος Ἀλέξιος ὁ Ὑπερασπιστὴς τῆς Ὀρθοδόξου Πίστεως. 7 Μαΐου. ΜΕΓΑΣ ΣΥΝΑΞΑΡΙΣΤΗΣ.
Makala hii bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari. |